CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa msimamo wake kuhusu mahusiano yanayolegalega kati ya Tanzania na Rwanda, huku kikitaka ukweli ujulikane na suluhu itafutwe ili nchi hizo jirani zisiingie katika vita.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA, ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana, Hezekia Wenje, aliwaambia waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam kuwa kuna ripoti zilizonukuliwa na gazeti la serikali ya Rwanda (News of Rwanda) kuwa waasi wawili wa Chama cha Rwanda National Congress (RNC), Dk. Theogene Rudasingwa na Condo Gervais pamoja na makamanda wa ngazi ya juu wa kikundi cha waasi wa FDLR walifanya kikao kilichoitwa cha malengo mahusi jijini Dar es Salaam.
Wenje aliongeza kuwa mratibu wa chama hicho, Condo Gervais pamoja na Rutasingwa waliwakilisha chama cha RNC huku Mtendaji Mkuu, Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi wakiwakilisha FLDR.
"Wiki moja kabla ya ripoti hiyo, gazeti la serikali ya Rwanda liliandika kuwa waziri mkuu wa zamani wa Rwanda, Faustini Twagiramungu, alikuwa nchini tangu Januari 19, 2014 kabla ya kusafiri kuelekea Lyon nchini Ufaransa ambako alitoa taarifa ya kikao cha Dar es Salaam mbele ya mkutano wa wajumbe wa chama chake na kupongezwa baada ya kusema sasa wapo tayari kuing'oa Serikali ya Rwanda hata kwa bunduki," alisema Wenje.
Wenje alisema kuwa gazeti hilo la Rwanda lilieleza pia kuwa Desemba 20 mwaka 2013, Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi walisafiri toka Tanzania kwenda Msumbiji kwa kutumia hati za kusafiria za Tanzania kwa mazungumzo na watu wanaodaiwa kuwa ni mamluki wa chama cha RNC.
Kutokana na taarifa hizo, CHADEMA ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini, kimeitaka serikali kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo, hasa zile za pasi za kusafiria na kujiridhisha kuwa jina la Tanzania halitumiki vibaya kwa kuhusishwa kuwafadhili watu ambao wanataka kuiondoa serikali iliyochaguliwa na wananchi wa Rwanda.
Pili, CHADEMA imelitaka Bunge kupitia Kamati ya Mambo ya Nje inayoongozwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kuunda kamati ndogo ili ifuatilie tatizo lililopo kati ya Rwanda na Tanzania ili ukweli ujulikane na mgogoro huo utafutiwe suluhisho mapema kuepusha vita inayoweza kutokea kwa nchi hizi jirani ambazo zote zipo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wenje aliongeza kuwa CHADEMA inataka kujua iwapo kama kuna maofisa wa juu wa Serikali ya Tanzania ambao kwa maelekezo au kwa sababu zao binafsi walishiriki katika utoaji wa hati za kusafiria kwa raia ambao si Watanzania kwani ni kosa kubwa katika mikataba ya kidiplomasia.
Tatu, CHADEMA kimeitaka serikali imwonye Twagiramungu ili abainishe kama alikuja Tanzania kufanya nini, na aeleze nia yake ya kusema kuwa alikuwa katika kikao mahususi hapa nchini, jambo ambalo limesababisha kusuasua kwa mahusiano ya nchi hizo mbili.
Hata hivyo, CHADEMA kimesema serikali imtake Twagiramungu afute kauli yake, aombe radhi Watanzania kwa kuharibu mahusiano ya Tanzania na Rwanda, na kuharibu sifa ya Tanzania kuonekana inafadhili waasi, jambo ambalo ni kinyume kabisa na mkataba wa Afrika.
No comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.